Alisema
yeye si wa kulaumiwa kutokana na wanafunzi hao kufanya vibaya kwenye
mtihani wa kidato cha nne na kwamba wanaosema waziri anapaswa kujiuzulu
hawana hoja za msingi zaidi ya kutaka kujipatia umaarufu kwa kudandia
hoja zinazokuwapo kwa wakati husika.
“Unajua
katika mfumo wa vyama vingi, kila linapotokea jambo baya basi wanaona
dawa ni kiongozi mhusika kung’oka. Unapozungumza waziri kujiuzulu hiyo
ni lugha ya kisiasa lakini hata akijiuzulu inakuwa bado tatizo
halijaweza kupatiwa ufumbuzi,” alisema.
Dk
Kawambwa alisema hata Serikali haijafurahishwa na matokeo hayo mabaya
na kushauri njia nzuri ni kutafuta dawa ya kukabiliana na tatizo la
wanafunzi kufeli huku akiahidi kuwa wizara yake inaangalia tatizo hilo
kwa karibu zaidi ili kujua chanzo chake.
Alisema
amesikitika kuona hata shule ambazo zilikuwa zinategemewa kufanya
vizuri zikiwamo za seminari, watu binafsi na kongwe za Serikali, nazo
zimefanya vibaya.
Aliunga mkono maoni ya kutaka mfumo mzima wa elimu nchini uangaliwe upya kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa elimu.
Lowassa
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Lowassa alisema matokeo hayo ni aibu kwa
taifa na kuilaumu Serikali kwa kuzitelekeza shule za sekondari za kata.
Alisema taifa kwa sasa linazalisha wabeba kuni na maji na siyo wasomi ambao wanaweza kushindana kwenye soko la ajira.
Alisema
sekondari za kata ambazo zilianzishwa chini ya usimamizi wake akiwa
Waziri Mkuu, zilikuwa ukombozi kwa Watanzania wengi wa kipato cha
kawaida na ndiyo sababu waliitikia wito kwa kuchangia ujenzi, hatua
ambayo alisema ilimpa faraja kubwa.
“Serikali
tuliahidi kuzikamilisha shule hizo kwa kuzijengea maabara na
kuhakikisha zina walimu. Ni wajibu wake kutimiza. Mimi ndiyo maana hata
kwenye Katiba Mpya nilipendekeza uwezekano wa elimu ya sekondari kuwa
bure, elimu ni kama mapigo ya moyo ya taifa ukiona hayaendi vyema lazima
ujiulize,” alisema.
Lowassa, ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008, alisema tangu aondoke madarakani, shule hizo nazo zimetelekezwa.
Alimwomba
Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua za makusudi, ikiwa ni pamoja na
kuunda tume ili ichunguze kwa makini kiini cha matokeo hayo mabaya.
“Matokeo
hayo ni aibu kwa taifa, walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe. Namwomba
kwa dhati Rais afanye kitu cha ziada, natambua mchango wa juhudi zake
katika sekta nyingine ikiwamo ujenzi wa barabara nchini lakini elimu
ndiyo iwe ya kwanza,” alisema.
Alitaka
ufike wakati nchi iamue kuwekeza katika elimu tofauti na ilivyo sasa
kwa Tanzania kuwa nchi inayotenga fedha kidogo zaidi katika sekta hiyo
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).